Pages

Wednesday, April 18, 2012

Milioni 70/- zatumika kumzika Kanumba



KAMATI ya mazishi ya aliyekuwa msanii maarufu nchini, Steven Kanumba, imesema imetumia Sh milioni 70 kugharimia maziko yaliyofanyika Aprili 10.

Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Aprili 7 na kuzikwa siku tatu baadaye kwenye makaburi ya Kinondoni na maelfu ya wananchi wa Dar es Salaam na mikoa jirani.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mtitu Gabriel alisema jana kwamba kamati hiyo iliyoratibu mazishi ya msanii huyo tangu Aprili 7, ilikusanya michango na ahadi za takribani Sh milioni 90 huku gharama za mazishi hadi maziko vikigharimu Sh 70,502,000.

Akitoa mchanganuo huo, Mtitu alisema Kamati yake ilitumia Sh 52,102,000 na ahadi za malipo ya vifaa ambazo ni Sh 18,400,000 na zilitumika kwa vifaa mbalimbali zikiwamo taa, jukwaa, viti na maturubai.

Alisema Sh milioni nne zilizobaki kutokana na zilizokusanywa zilikabidhiwa kwa mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa na Kamati haijatimiziwa ahadi ya Sh milioni 15.5.

Alipoulizwa kama Kanumba ameacha mali ya Sh milioni 700, Mtitu alisema pamoja na msanii huyo kuwa na jina kubwa, lakini alikuwa masikini na si tajiri kama ilivyokuwa inafikiriwa.

“Pamoja na jina la Kanumba kuwa kubwa, hakuwa na fedha, na ndiyo maana baada ya kutoka kuhifadhi mwili wake Muhimbili, tulijikusanya na kujipanga kuhakikisha tunampumzisha kwenye nyumba ya milele kwa heshima ya hali ya juu na hili tumelifanikisha,” alisema Mwenyekiti huyo.

Pamoja na kukanusha ‘kuchakachua’ fedha zilizokusanywa, Mtitu alisema Kamati yake ilianza ikiwa haina hata Sh 100 na kulazimika wanakamati kubeba gharama za awali.

“Tulitambua mchango mkubwa wa Kanumba enzi za uhai wake, tuliona iko haja ya kufanya yote haya, tulianza tukiwa hatuna hata Sh 100, ingawa baadaye Kamati ilichangia gharama za awali ambazo zilipatikana miongoni mwa wajumbe wenyewe,” alieleza.

Akizungumzia kushindwa kutoa nafasi kwa wananchi kuaga mwili wa Kanumba, Mtitu alisema Kamati ilikadiria kuwa watu wapatao 40,000 wangehudhuria kutokana na idadi ya watu ambao walikuwa wakifika msibani, lakini wingi wa watu na ufinyu wa muda siku hiyo ndivyo vilifanya utaratibu ukatizwe.

“Wakati wa mazishi tulikuwa tunahudumia waombolezaji 3,000 mpaka 4,000 kwa siku, hivyo tukaweka makadirio ya watu 40,000 siku ya maziko, lakini watu waliojitokeza walikuwa wengi na ikawa vigumu kutoa nafasi kwa wote kuaga, hasa kutokana na wingi na mazingira yalivyokuwa na muda pia,” alifafanua.

Kamati iliyoratibu shughuli zote za mazishi iliundwa na wadau wa filamu, wasanii, wafanyabiashara, ndugu na marafiki wa Kanumba, aliyekuwa mwigizaji nyota wa filamu nchini na aliyevuma pia katika nchi mbalimbali barani Afrika.

Kifo chake kilikuwa cha utata baada ya kudaiwa kuwa na ugomvi na mwigizaji wa kike, Elizabeth Michael ‘Lulu’, ambaye inadaiwa alikuwa mpenzi wake.

Lulu tayari amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa tuhuma za mauaji ya msanii huyo.

Katika hatua nyingine, Gabriel alisema katika kumuenzi Kanumba, wanafikiria kuandaa Tuzo za kutambua kazi za sanaa ya maonesho na filamu, ambazo wataziita kwa jina la Tuzo za Steven Kanumba.

CHANZO: HABARI LEO
:) :( ;) :D ;;-) :-/ :x :P :-* =(( :-O X( :7 B-) :-S #:-S 7:) :(( :)) :| /:) =)) O:-) :-B =; :-c :)] ~X( :-h :-t 8-7 I-) 8-| L-) :-a :-$ [-( :O) 8- 2:-P (:| =P~ #-o =D7 :-SS @-) :^o :-w 7:P 2):) X_X :!! \m/ :-q :-bd ^#(^ :ar!

No comments: