Pages

Monday, August 29, 2011

i admire this woman today

SUSAN MASHIBE; Rubani, Mhandisi wa Ndege,Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni mbili zinazoshughulika na masuala ya anga
Susan ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi wa Kampuni ya TanJet, kampuni ya ya kimataifa na ya kwanza ya aina yake nchini inayoshughulikia masuala ya kiufundi katika ndege binafsi, za biashara na hata za kidiplomasia
pia ni mmiliki kampuni nyingine inayojulikana kama Kilimanjaro Aviation Logistic Center, ambayo inashughulikia taratibu za utuaji na urukaji wa ndege binafsi katika Bara la Afrika.
Susan ni mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki mwenye Cheti cha Rubani cha FAA na Mhandisi Matengenezo wa Ndege. Tangu kuanzisha TanJet mwaka 2003, Mashibe ametunukiwa Tuzo mbalimbali ikiwemo ya Askofu Desmond Tutu ya mwaka 2009 na ile ya Mwanamke Mjasiriamali mwenye Mafanikio ya mwaka 2009.

Ndoto ya Susan ya kutaka kurusha ndege haikuanza wakati akiwa chuoni la hasha! bali akiwa na umri wa miaka minne tu ndipo alipogundua sehemu inayomfaa ni kwenye `mawingu’. Anasema,“ nilizoea kuwaona wazazi wangu na ndugu zangu wakipanda ndege na kuondoka, wakiniacha.

Wakati huo tulikuwa tukikaa Kigoma na walikuwa wakirudi Dar es Salaam, na niliachwa na bibi. “Nilipokuwa nikiangalia ndege ikiondoka nikawa nafikiria kama ningekuwa najua kurusha ndege nisingeachwa tena,” anasema Susan ambaye ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto sita.

Wakati huo wote, Susan alikuwa na shauku kufahamu ni kitu gani cha kufanya ili mtu awe rubani, na kufahamu namna ndege inavyofanya kazi. Anaendelea kusema kuwa, “bado nakumbuka hisia nilizopata nilipoona Ndege ya Shirika la Ndege ya Uingereza aina ya Boeing 737 kwa mara ya kwanza, nilikosa maneno ya kusema, nilikuwa sijaona kitu kizuri na kikubwa kama kile, lakini kilichonivutia zaidi ni namna ndege inavyoanza kuruka.”

Hisia alizopata Susan ziligeuka kuwa mapenzi na kitu cha kuvutia ambavyo vilimtawala binti huyo tangu akiwa mdogo. Mapenzi yake yalitimizwa zaidi pale mjomba wake alipompeleka kwenda kutembea uwanja wa ndege wakati alipokwenda Dar es Salaam kumtembelea akiwa na umri wa miaka 10.

Kila mtu katika familia yake alifahamu malengo ya binti huyo. Kwa hiyo haikuwa kazi ngumu kwa Susan kumshawishi baba kubariki kazi aliyoichagua baada ya kumaliza Kidato cha Nne. “Nilichaguliwa kujiunga na ualimu, lakini baba aliyekuwa mfanyakazi wa umma aliniuliza nataka kufanya nini. Nikamwambia nataka kuwa Rubani, kisha akaniambia timiza ndoto yako.”

Hivyo kweli Susan ametimiza ndoto yake. Mwaka 1993 alianza kozi ya Uhandisi wa Ndege katika Chuo cha South Western Michigan nchini Marekani ambapo dada yake alikuwa akiishi. Baba yake alimshauri kuchukua kozi hiyo nchini Marekani na alilazimika pia kujifunza lugha ya Kiingereza.

“Niliambiwa siwezi kuwa rubani kama sizungumzi Kiingereza kwa sababu nitatakiwa kuwasiliana na mnara wa kuongozea ndege,” anasema. Hata hivyo, mwaka 1995 mambo yalikuwa magumu baada ya familia yake nyumbani Tanzania kusema haiwezi kumsaidia kielimu kutokana na matatizo ya kifedha.

“Kwa muda nilifikiria ndoto yangu imekufa…nilipoteza matumaini, hamu ya kula na matokeo yake niliumwa.” “Nililazwa hospitalini na wakalazimika kunirudisha nyumbani ili nipate nguvu, jambo ambalo nilifanya. Lakini nikiwa nyumbani nilitafuta ufumbuzi wa muda mrefu kuwa kuanzia sasa sitamtegemea mtu ila mimi mwenyewe, niliamua nitarudi kumaliza shule na nitarusha ndege mwenyewe.”

Hicho ndicho alichofanya. Kwa namna fulani alirudia hatua zake na kurudi shule na alihitimu mwaka 1996. Mwajiri wake wa kwanza ilikuwa Kampuni ya Duncan Aviation, iliyokuwa mjini Michigan, Marekani. Susan alianza kazi ya ukaguzi mkubwa katika ndege kadhaa za kibiashara.

“Nilianza masomo ya kurusha ndege katika Chuo Kikuu cha Western Michigan, nikisimamia zaidi katika ndege. Ilikuwa gharama kubwa, na nililazimika kufanya kazi saa nyingi usiku ili niweze kuhudhuria darasa, “ anasema.

Lakini bahati nzuri alikuwa akichukua masomo katika kampuni yake kwa hiyo alilipa nusu ya ada, faida ambayo mwajiri alikuwa akitoa kwa wafanyakazi wake. Mwaka 2002, Susan alipata cheti cha kutambuliwa kufanya kazi katika ndege za biashara, baada ya kumaliza Shahada ya Kwanza ya Utawala wa Mambo ya Anga.

Hata hivyo, maisha yalianza kuwa magumu kwa yeyote aliyeko katika biashara ya ndege kwa sababu ya tukio la mashambulizi ya kigaidi Septemba 11, 2001 nchini Marekani. “Baada ya tukio la Septemba 11, mashirika ya ndege yalipata misukosuko, watu walikosa huduma.

Ilikuwa kazi ngumu, baadhi ya kampuni zilifungwa, kwa hiyo nikaamua nyumbani ndipo natakiwa kuwepo,” anasema. Susan alishajinyima sana na kuweka akiba ya kutosha kurudi nayo nyumbani kwa ajili ya kuanzisha biashara yake.

Kwanza alifikiria kutafuta ajira, lakini kampuni nyumbani Tanzania zilisema elimu yake iko juu sana. Hakuwa na chaguo lingine zaidi ya kutumia akiba yake na kukodi chumba chenye ukubwa wa mita za mraba 13 tu katika Uwanja wa Ndege ambapo alifungua kampuni yake Julai 1, 2007.

“Kila mtu alidharau uamuzi wangu, wakiniambia muda wa miezi mitatu tu nitakuwa nimefunga ofisi, lakini nipo mpaka leo,” anasema na kueleza namna biashara yake inavyolipa. Mteja wake wa kwanza alikuja siku 20 baada ya kufungua biashara yake na alikuwa Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ambaye alifika kutembelea Tanzania.

Washirika wake walioko Afrika Kusini walimuunganisha na kazi ya kuhudumia ndege ya Zuma. Ilikuwa ni hatua kubwa kwake kupata tenda hiyo ya kusimamia ndege zote zilizopo chini ya Ubalozi wa Marekani.

Wakati akifurahia mafanikio hayo makubwa, Susan anasema furaha yake ilikuwa alipoweza kulipa kodi inayofikia kiasi cha Sh milioni 500 kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Ulikuwa mchango mkubwa uliowashtua wengi. Kama ilivyo kwa wanawake wengi wanapofanya kazi zilizotawaliwa na wanaume zaidi naye amekumbana na vikwazo.

Baadhi ya watu walidharau kwa kumuangalia tu. Anakumbuka aliwahi kuzuiwa kuingia katika ndege ya kidiplomasia kwa sababu walinzi walidhani hana shughuli ya kumuingiza humo. Lakini baadaye walishtuka walipobaini kuwa mwanadada huyo ndio alipewa jukumu la kusimamia ndege hiyo.

“Mimi ni mwanamke, navaa viatu virefu, napaka vipodozi na mambo mengine kama hayo, kwa hiyo rubani anapoangalia na kuona mimi ndiye ninafanya kazi ya kuhudumia ndege yao hushtuka na kudhani sina uwezo huo, wengine hunisimamia ninapofanya kazi, lakini sura zao hubadilika wanapobaini ninachoweza kufanya,” anasema.


:) :( ;) :D ;;-) :-/ :x :P :-* =(( :-O X( :7 B-) :-S #:-S 7:) :(( :)) :| /:) =)) O:-) :-B =; :-c :)] ~X( :-h :-t 8-7 I-) 8-| L-) :-a :-$ [-( :O) 8- 2:-P (:| =P~ #-o =D7 :-SS @-) :^o :-w 7:P 2):) X_X :!! \m/ :-q :-bd ^#(^ :ar!

1 comment:

Anonymous said...

Hi therе! I јust wanted to ask if уou еver
have any issues with hackeгs? Μy last blog (ωоrdprеss) was haсκeԁ anԁ I endеd
up losing many months of hard work due tο no back up.
Do you haѵe any solutions to ρrеvent hаcκеrs?


My web page :: http://idrotherapyreviews.com/
Feel free to surf my site :: http://idrotherapyreviews.com,http://idrotherapyreviews.com/,http://www.idrotherapyreviews.com/,http://www.idrotherapyreviews.com, www.idrotherapyreviews.com, www.idrotherapyreviews.com/